Pages

KARIBU NASHERA HOTEL, MOROGORO - | Boma Road, LITI Area P.O. Box 237, Morogoro | Tel. +255 23 26139

Feed icon

Monday, June 23, 2014

NEY UNASTAHILI PONGEZI, WENGINE WAJIFUNZE KWAKO!
KWAKO,
Staa wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’. Mambo vipi kamanda? Habari za mishe za town? Bila shaka mambo yanakwenda poa kabisa na mchakamchaka wa maisha unaendelea kama kawa.
Kama ndivyo ni vyema. Kwa upande wangu nakwenda sawa, changamoto za hapa na pale kama kawaida, kwenye maisha hazikosekani.
Leo nimekukumbuka kwa barua. Najua kidogo utakuwa umeshtuka, maana wengi wanaamini barua zangu zina lengo la kuponda tu. Si kweli. Barua ni uwanja wa kupeana ukweli.
Staa anapofanya jambo baya anakumbushwa lakini akifanya kitu kizuri, husifiwa na kupewa moyo. Ney nimekupata kukufahamu kwa kipindi kifupi sana kwenye game ya Bongo Fleva.

MWANAMKE WAKO AMEKUWEKA KUNDI GANI?


KATIKA mapenzi kuna mambo mengine yanaumiza lakini ni vizuri kujifunza. Ukijua inakuwa rahisi kukaa nayo mbali.
Kuna kitu nataka kukupa rafiki yangu mpendwa. 
Je, unajua kuwa baadhi ya wanawake huwaweka wanaume katika makundi? Ndugu zangu baadhi ya wanawake wasio waaminifu wenye wanaume zaidi ya mmoja huwaweka wanaume kwenye makundi matatu.
Unaweza kuwa na msichana mkapendana sana, kwa sababu ya upofu wa mapenzi usijue amekuweka kundi lipi. Ni vizuri kuyafahamu makundi hayo kisha kujichunguza ili ujue kundi ulilopo.

Wednesday, June 11, 2014

EMMANUEL, FLORA MBASHA, NINI KIPO NYUMA YENU?
KWENU,
Emmanuel na Flora Mbasha. Naamini afya zenu zipo sawa na mnaendelea kuhangaika na maisha ingawa kuna changamoto zimeingia kati yenu. Napenda kuwahakikishia kuwa, hayo ni mapito tu. Yataisha.
Naandika barua hii hasa kwa msukumo wa imani yangu ambayo nanyi mnaiamini. Kwangu mimi kama Mkristo, ninyi ni viongozi wangu wa kiroho. Sina shaka na hilo hata kidogo.
Ni viongozi wa Wakristo wengi ndani na nje ya nchi. Nasema hivyo kwa sababu ninyi ni Wainjilisti, mnaotangaza neno kupita uimbaji! Mmebadilisha maisha ya wengi kwa kupitia nyimbo zenu.
Kwa msingi huo sina shaka yoyote wala siogopi kuwaita viongozi wa dini, kwa kuwa mmesimama mbele ya Wakristo na kuwatangazia habari njema kupitia nyimbo zenu.
Hivi sasa kuna jambo limezagaa na kuwachafua sana. Sitapenda kulizungumzia sana hilo, maana ni jambo ambalo bado linaonekana kuwa na makengeza lakini pia lipo kwenye mikono ya sheria.
Hata hivyo, sakata hilo linalomhusisha Emmanuel Mbasha na ubakaji halijafika mahakamani, hivyo bado linajadilika. Lakini sitafanya hivyo. Kuna mambo nataka kuwashauri kuhusu ndoa yenu.
Kinachonifanya niwaandikie barua ni namna sakata hilo lilivyo na hali ya ndoa yenu kwa sasa. Kwanza kabisa, inaonekana mlikuwa na mgogoro kwa muda mrefu hadi kufikia Flora kuondoka nyumbani na kwenda kuhamia hotelini!

Thursday, April 3, 2014

UTAPOTEZEWA MUDA WAKO HADI LINI? - 3KUJIFUNZA, kuelewa na kufuata ni kitu kizuri kwa mtu mwenye hulka ya kupanua mawazo yake. Hakuna aliyekamilika, siku watu wanakosea. Hakuna mtaalamu wa kudumu wa mapenzi.
Kwenye mapenzi tunazidiana uelewa tu. Hapa kwenye All About Love, ni mahali sahihi pa marafiki kukutana na kubadilishana mawazo. Wengi wamenufaika kwa kuwa wadau wa kona hii.

Ni safu ya kitambo iliyobadilisha fikra za wengi. Nashukuru wale ambao wananishirikisha mafanikio yao ya kimapenzi baada ya kusoma mada zangu na kuzifanyia kazi.
Marafiki, leo nahitimisha mada hii kabla ya kuanza kuchambua mpya wiki ijayo. 

Ni kuhusu wanawake wanavyopotezewa muda na wanaume ambao hukaa nao muda mrefu katika uchumba unaishia hewani.
Nilifafanua kwa undani mambo mawili; kuachwa kwa muda mfupi na wanaume tofauti – nikaeleza sababu na namna ya kufanya. Pia nilifafanua kuhusu kuachwa kwa wasichana baada ya kukaa muda mrefu kwenye uhusiano.

EXCLUSIVE - BATULI: IRENE UWOYA ALICHUKUA NAFASI YANGU KWA KANUMBAMakala: Joseph Shaluwa
NI nadra sana kumkuta akiwa amenuna. Sura yake mara zote ni yenye tabasamu, uso wake una nuru na angavu wakati wote. Macho yake ni kivutio kingine kwa mrembo huyu. Weka yote pembeni, kutana naye akiwa nyuma ya kamera utamkoma!

Maneno ya kuanisha sifa zake ni mengi. Naweza kuandika ukurasa mzima, lakini hayo yatoshe kueleza ubora wa mwananadada huyu katika uhalisia na uigizaji. Ni Batuli.
Jina lake halisi ni Yobnesh Yusuph, 28, mama wa watoto wawili, wavulana – Samir na Malima. Katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya, Batuli amezungumza mengi kuhusu maisha yake na changamoto anazokutana nazo kwenye sanaa.

Kwanza nilitaka kujua kwa nini kumekuwa na migogoro ya wasanii wa kike kuchukuliana mabwana? Huyu hapa anafafanua: “Wanaoweza kufanya hivyo ni wenye tabia za aina hiyo tu. Ni kweli kuna hiyo tabia miongoni mwetu lakini kiukweli inashusha sana heshima.
“Matokeo yake sasa, hata sisi ambao hatuna tabia hizo, tunawekwa kwenye mkumbo mmoja. Lakini sababu hasa ninayoiona ni tabia ya sisi wanawake kutambiana. Mtu akiwa anatoka na mwanaume fulani anaanza kumwanika na kueleza sifa zake.

“Sasa waroho ndiyo wanapoanza kummnendea na wakimkwapua, inakuwa imekula kwako. Ndiyo maana mimi nimeamua kamwe sitamweka wazi mwanaume ninayetoka naye hadi itakapofikia hatua ya ndoa. Ni kwa sababu naogopa majanga kama hayo."

Vipi maisha yako ya ndoa?
“Niliwahi kuishi na mume wangu wa ndoa, tukafanikiwa kupata mtoto mmoja, lakini baadaye ilibidi nidai talaka. Niliishi kwenye ndoa ya manyanyaso sana. Mume wangu alikuwa akinisaliti waziwazi kiasi kwamba alifikia hatua akawa anatoka na marafiki zangu wa karibu.

Friday, March 28, 2014

UHUSIANO: NI RAHISI KUIMARISHA NDOA YAKO!
ILI uwe na ndoa yenye furaha ni lazima utenge muda wa kutafakari namna ya kuiboresha na kutafuta furaha ya ndoa hiyo. Ndugu zangu, kila kitu kinatengenezwa.
Waswahili wanasema, ukiona vyaelea, ujue vimeundwa. Huwezi kuacha mambo yakajiendesha hovyo ukategemea kuwa na ndoa bora. Uhusiano imara unakutegemea wewe.
Kila mmoja ana wajibu wa kuangalia furaha ya mwenzake. Yapo mambo mengi muhimu ambayo kama wanandoa wakiyafanya huboresha uhusiano wao, lakini hapa nitakutajia yale muhimu zaidi.

ISHI KIRAFIKI
Kuna baadhi ya wanandoa wakishaingia kwenye muunganiko huo, ule urafiki uliokuwa zamani wakati wa uchumba, hilo ni tatizo. Ukitaka kuwa na ndoa yenye furaha lazima umfanye mwenzi wako kama rafiki yako.
Baadhi ya wanaume wana tatizo la ubabe na kujiona kuwa wao ni wanaume hivyo hawapaswi kuguswa kwa lolote. Ndoa inageuka jeshini. Hilo ni tatizo.

Mshirikishe mwenzako kwenye mambo yako. Kuwa na kauli njema muda wote. Sikiliza shida za mwenzako na namna ya kuzitatua. Sikiliza pia hisia zake.
Usipoishi naye kirafiki, maana yake ataogopa hata kukueleza mambo fulani ya msingi ambayo labda havutiki nayo. Ukimsogeza kama rafiki atakueleza mambo ambayo hayamfurahishi.

LOVE STORY: PENZI SHUBIRI - 2MTUNZI: JOSEPH SHALUWA

ILIPOISHIA JANA...
Baada ya kufanya mipango yote kwa siri, tuliamua tukapumzike Marangu Mtoni, twende huko siku ya week-end tukafurahie maisha!
Kila nikiufikiria uzuri wa Linna nazidi kuchanganyikiwa, siyo siri Linna ni mrembo jamani! Tamaa ya mapenzi ilinizidi, mshawasha wa mapenzi ukanipanda nikaamua kumweleza hisia zilizoko katikati ya moyo wangu.
Mwanzo niliogopa, lakini nijipa moyo nikamweleza. Cha ajabu sasa, wala hakukataa, alikuwa maharage ya Mbeya! Maji mara moja! Akadai eti alikuwa ananipenda mimi tu na alikuwa na Shams kwa sababu ya kitu kimoja tu; pesa! Si vinginevyo.
Mh! Jamani nyie!!!
SASA ENDELEA...

KWANZA tulienda kushangaa maporomoko ya maji kwenye milima iliyokuwa jirani na hoteli tuliyofikia. Tulipata upepo na hewa safi ya mlima Kilimanjaro. Kaubaridi ka eneo hilo kalikuwa si mchezo!
Baada ya hapo tukaingia maeneo ya chini kabisa ya maporomoko ya maji yale, ambapo kulikuwa na vijito vidogovidogo. Tukaanza kuchezea maji ambayo yalikuwa baridi kabisa.

Tuliufurahia uumbaji wa Muumba wetu!
Kweli ashukuriwe!
Hapo tulipokuwepo hapakuwa mbali sana na geti la kuingilia mlima mrefu kuliko yote Afrika - Kilimanjaro. Tulikuwa kilomita chache sana karibu na mwanzo wa mlima maridadi ambao tunajivunia kuwa nao na unauingizia nchi yetu fedha za kigeni kila kukicha. 

Penyewe paliitwa Kilimanjaro National Park.
Baada ya kuridhika na utalii feki wetu, tuliongozana moja kwa moja mpaka Marangu mtoni darajani; tukapanda barabara ya kuelekea Kilema.
Kwa umbali kidogo tukaona jengo moja la ghorofa mbili, tukalipenda, baada ya kulichunguza kwa muda tuling’amua ilikuwa hoteli. Ilikuwa karibu na Chuo cha Ualimu cha Marangu. Sikumbuki vizuri jina la hoteli hiyo lakini tuliingia na kutafuta mahala pazuri patakapofaa kwa ajili ya mazungumzo.

Macho yetu yalipata burudani ya kuangalia maua ya kila aina ya liyokuwa kila kona ya ile hoteli. Burudani ambayo hatukuilipia gharama yoyote.
“Pazuri sana hapa, nadhani patatufaa sana kwa ajili ya mazungumzo au vipi?” nilimwambia Linna huku nikisogelea sofa moja kubwa lililokuwa karibu na pale tulipokuwa.
”Sawa mpenzi, hakuna tatizo,” aliniambia.

Thursday, March 27, 2014

LOVE STORY: PENZI SHUBIRIMTUNZI: JOSEPH SHALUWA

Sehemu ya Kwanza

Julai 22, 2004 – Moshi, Kilimanjaro.
NILIKUWA nimejilaza kwenye sofa kubwa, nikiwa nimevaa bukta yangu nyepesi na flana ya kukata mikono, kifuani mwangu kulining’inia cheni ya dhahabu iliyong’ara barabara, huku macho yangu nikiwa nimeyaelekeza kwenye TV yangu kubwa ya rangi iliyokuwa pale sebuleni kwangu, iliyokuwa inaonyesha mwanadada mrembo Celine Dion na wimbo wake wa I’m Alive. Wimbo huo kipenzi changu cha moyo wangu, Josephine alikuwa anaupenda sana. Nikatamani atoke mapema huko bafuni ili auone na kuusikiliza.

Ghafla simu ya mpenzi wangu, Josephine ambayo ilikuwa pale mezani iliita! Sikung’amua mara moja kuwa ilikuwa ni simu au ni ujumbe mfupi wa maneno. Kwa kuwa mimi na mpenzi wangu Josephine tunaaminiana, niliamua kuiendea simu ili nipokee!
Baada ya kuifikia niligundua ilikuwa siyo simu bali ni ujumbe mfupi wa maneno. Ilikuwa ni kawaida yetu kila mmoja kuangalia simu ya mwenzake, kutokana na sababu hiyo, sikuona woga kufungua ule ujumbe mfupi uliokuwemo na kuanza kusoma.

Kila nilipomaliza kusoma neno moja, ndivyo jazba ilivyozidi kunipanda. Nusura nipate uchizi. Uso wangu ulikuwa umechora makunyanzi makubwa mithili ya matuta kutokana na jazba iliyokuwa inaendelea kunipanda kila nukta moja ilipoondoka.
Sikuamini yaliyotokea kuwa ni kweli au nilikuwa ndotoni, nilikuwa naombea iwe ndoto na sio kweli. Hasira ikanijaa. Unaweza kudhani labda ni hadithi ya kufikirika, lakini haikuwa hivyo bali ilikuwa ni ukweli halisi.

“Shit…! Huyu mpuuzi ananitania siyo? Ngoja atoke huko bafuni,” niliwaza.
Nilikaa kimya nikiwa nimeishikilia ile simu, nisijue la kufanya. Niliduwaa. Nikawa namsubiri kwa hamu sana atoke bafuni ili anieleze vizuri.

NIMEBALEHE, SIJAWAHI KUFANYA MAPENZI, NITADHURIKA?SHIKAMOO kaka Shaluwa. Mimi ni msichana mwenye miaka 22. Sijawahi kufanya mapenzi. Kuna mwanaume nilikuwa naye lakini tuliachana. Nataka mwanaume atakayenitoa usichana wangu awe mume wangu wa ndoa. Tatizo rafiki zangu  wanasema eti nitapata matatizo. Ni kweli?
Tegnelila, Moro.

NASAHA: Marhaba mdogo wangu. Hakuna tatizo la Kibaolojia linalosabishwa na kutokufanya mapenzi kwa mtu ambaye hajawahi kushiriki. Mwanamke kuwa na usichana wake hadi ndoa ni heshima kwa jamii yetu ya Kiafrika.
Hata hivyo, inakupasa uushughulishe mwili wako kwa mazoezi madogomadogo ili kujiweka kando na maudhi ya hapa na pale ambayo yanaweza kujitokeza kutoka na kutoshiriki tendo hilo.
***

Nimeachwa lakini anawasiliana na rafiki yangu
Kaka Joseph, hongera kwa kazi. Mimi ni binti mwenye miaka 20. Nimeachwa na mpenzi wangu hivi karibuni, kisa eti sikupokea simu yake. Bado nampenda sana. Lakini kinachonishangaza ni kwamba anawasiliana na rafiki yangu kipenzi. Kuna nini? Naomba msaada wako.

NASAHA: Pole kwa matatizo. Mapenzi ni sawa na uwekezaji. Yaani umpende mtu anayekupenda. Mwenzako hakuwa na sababu ya msingi ya kukuacha. Kwa maana hiyo, huyo mwanaume hakuwa na malengo na wewe ndiyo maana alikuwa anatafuta sababu ya kuachana kwenu. Rafiki yako naye anaonekana kukusaliti.
Tuliza moyo, angalia ustaarabu mwingine. Kuanza upya siyo ujinga.

NAWE KAMA UNA SWALI, UNAWEZA KUANDIKA HAPA KWENYE MAONI AU EMAIL JOESHALUWA@GMAIL.COM. KARIBUNI.